Back to top

KUNENGE AIPONGEZA DAWASA, AWAPA JUKUMU MADIWANI

17 March 2026
Share

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bw. Abubakar Kunenge, amesema ushirikishwaji wa wananchi kwenye miradi ya maendeleo unaofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ni wa mfano na unapaswa kuigwa na taasisi zingine.

RC Kunenge amesema hayo wakati akizindua rasmi ziara ya kimafunzo kwa Madiwani wa Mkoa wa Pwani, ya kutembelea vyanzo vya maji na mitambo ya kuzalisha maji ili kupata uelewa wa pamoja wa hatua za uzalishaji hadi kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.

Aidha, amewaomba Madiwani kutoa ushirikiano kwa DAWASA ili kuhakikisha wananchi wanatunza vyanzo vya maji na kupitia Halmashauri zao nao wanatenga fedha katika bajeti kwa kuweka kipaumbele miradi ya maji ilikupunguza tegemeo lote kwa DAWASA na kuweza kufanikisha utelekezaji wa miradi mingi ya maji.

Amesema ziara iliyoandaliwa na DAWASA ni kielelezo muhimu cha ushirikishwaji wa wananchi ili kuwa na mipango ya pamoja katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Kunenge amesema DAWASA inapata fedha kutoka Serikali kuu, hivyo utatuzi wa changamoto unakuwa kwa mkakati, lakini amesema kwenye Serikali za Mitaa pia zitengwe fedha kwa ajili ya miradi ya maji li kuipunguzia mzigo DAWASA.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema mkakati uliopo kwa sasa ni kuwashirikisha wadau muhimu wakiwemo Madiwani ambapo wameanza na Mkoa wa Pwani kwa kuwaandalia ziara na baadaye kutembelea kila Halmashauri kwa ajili ya mafunzo kuhusiana na huduma ya maji pamoja na upangaji wa  vipaumbele vya kutekeleza.