
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema uzinduzi wa meli ya kwanza ya uvuvi wa bahari kuu ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ni hatua ya kimapinduzi inayolenga kuimarisha uchumi wa taifa kupitia sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Kigamboni jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema serikali imejipanga kikamilifu kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa kutumia rasilimali za bahari kuu ambazo kwa muda mrefu hazikutumika ipasavyo na kwamba uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuongeza tija katika sekta ya uvuvi, huku ukilenga kuunganisha shughuli za uzalishaji, uchakataji na masoko ya samaki ndani na nje ya nchi.
Rais Samia amesisitiza kuwa serikali ina dhamira ya kulifufua na kuliimarisha Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ili liwe chombo imara kitakachosaidia taifa kunufaika kikamilifu na rasilimali za bahari kuu, na juhudi zinaendelea kuimarisha udhibiti wa rasilimali za maji kwa kupambana na uvuvi haramu unaosababisha uharibifu wa mazingira na kupunguza rasilimali za samaki.
Katika kuhakikisha sekta hiyo inakua kwa kasi, Rais Samia amesema serikali imewekeza katika kuboresha mazingira ya uvuvi ikiwemo kuwezesha upatikanaji wa vifaa, utaalamu na mitaji pamoja na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa kama ufugaji samaki kwa njia ya vizimba.
Ameongeza kuwa mpango wa kununua meli nyingine nne pamoja na kuanzisha miundombinu ya mafunzo na utafiti ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kujenga uwezo wa taifa katika uvuvi wa bahari kuu, hatua hiyo inaendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 hadi 2050 pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025 hadi 2030, ambayo inalenga kujenga uchumi imara na shindani.
Ametoa wito kwa Watanzania na sekta binafsi kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya uvuvi, huku serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia uwekezaji zaidi na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu nchini, akieleza kuwa mafanikio ya mipango yote ya maendeleo yanategemea hali hiyo.
