Back to top

VYAMA 12 VYAUNGA MKONO RIPOTI YA TUME YA JAJI CHANDE

27 April 2026
Share


Vyama 12 vya siasa nchini vimejitokeza kwa pamoja kupongeza ripoti ya Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, na kutaka kuharakishwa kwa mchakato wa maridhiano pamoja na kupatikana kwa Katiba mpya kama ilivyopendekezwa na tume hiyo.

Vyama hivyo katika tamko lao la pamoja vimesema pendekezo la kuanza mchakato wa Katiba mpya kabla ya mwaka 2028 linapaswa kuchukuliwa kwa uzito, kwa kuwa linaweza kuwa suluhu ya changamoto za kisiasa na kijamii zinazoikabili nchi.

Vyama vilivyoshiriki kutoa tamko hilo ni DP, NRA, NLD, AAFP, ADA-TADEA, Demokrasia Makini, UPDP, UDP, SAU, UMD, TLP na CCK.

Vyama hivyo vimesisitiza utayari wao kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mapendekezo yote yaliyoainishwa na tume hiyo, kama sehemu ya kudumisha amani na utulivu pamoja na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo nchini.

Akizungumza kwa niaba ya vyama hivyo, Hassan Doyo, mgombea urais wa NLD katika uchaguzi Mkuu wa 2025, amesema kupatikana kwa Katiba mpya hakutaondoa tu changamoto za kisiasa bali pia kutasaidia kuliponya Taifa kutokana na changamoto mbalimbali linazopitia.

"Nchi itaendelea kuwa ya amani na yenye utulivu kupitia mchakato wa maridhiano na upatikanaji wa Katiba mpya," amesema Doyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jukwaa hilo na mgombea urais katika uchaguzi Mkuu wa 2025, Abdul Muya, ameipongeza Tume ya Jaji Mohamed Othman Chande na kutoa wito wa kuitishwa kwa Baraza la Vyama vya Siasa ili kujadili masuala mbalimbali yaliyoainishwa kwenye ripoti hiyo.

Aidha, amesisitiza vyombo vya dola kuanza kuchukua hatua dhidi ya vichocheo vilivyotajwa kama sababu ya ghasia zilizotokea Oktoba 2025.

Wakati wa hotuba yake baada ya kupokea ripoti hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza ahadi yake ya kupatikana kwa Katiba mpya katika kipindi chake cha pili cha uongozi, pamoja na kutangaza kuundwa kwa Tume ya maridhiano hivi karibuni itakayoratibu mchakato wa kufanikisha maridhiano nchini.