Back to top

KAPINGA: SERIKALI ITAENDELEA KUWAWEZESHA VIJANA WANAOWEKEZA

29 June 2026
Share

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe Judith Kapinga (Mb.), amesema Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele vijana wanaothubutu kuwekeza katika biashara, akimtaja mwanzilishi wa kinywaji cha KIX, kuwa mfano wa vijana wanaopaswa kuungwa mkono kwa kuamini fursa zilizopo nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kinywaji cha KIX,  Waziri Kapinga amesema   Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza mageuzi makubwa ya kisera, kisheria na kiutawala yaliyobooresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kupunguza urasimu, kufuta baadhi ya tozo zisizo za lazima na kuimarisha huduma za kidijitali, hatua zilizoongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kapinga amesema sekta binafsi inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi kwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya ajira rasmi na zaidi ya asilimia 90 ya ajira zote nchini, huku serikali ikiendelea kujenga uchumi shindani unaotegemea uzalishaji wenye thamani kubwa kupitia uwekezaji katika viwanda, biashara, kilimo na uchumi wa kidijitali.

Aidha, ameipongeza Amount Group Limited kwa kuwekeza nchini na kueleza kuwa mpango wake wa kujenga kiwanda cha uzalishaji ni ishara ya imani kwa mazingira mazuri ya biashara yaliyopo Tanzania.

Amewahimiza wafanyabiashara kuzingatia sheria, viwango vya ubora, utunzaji wa mazingira na kutekeleza wajibu kwa jamii ili kujenga biashara endelevu na zenye ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi. 

Pia amewataka Watanzania kuipokea bidhaa hiyo, akisema ushindani huongeza ubora wa bidhaa, ajira na mapato ya taifa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Amount Group Limited, Justine Ishengerema amesema uzinduzi wa KIX nchini si kuingiza bidhaa mpya pekee, bali ni mwanzo wa utekelezaji wa mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha uzalishaji nchini Tanzania.

Amesema kampuni inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa KIX katika Afrika Mashariki na Kati, huku ikiahidi kulipa kodi kwa wakati, kuzalisha ajira na kuzingatia sheria zote za nchi.