
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Prof. Mohammed Ali Sheikh, ametembelea banda la Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya Wizara.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea maandalizi yaliyofanyika katika mabanda ya taasisi mbalimbali pamoja na kujiridhisha na ubora wa huduma na elimu inayotolewa kwa wafugaji, wavuvi na wananchi wanaotembelea maonesho hayo.
Akiwa katika banda la TVLA, Prof. Sheikh alipokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Wakala kutoka kwa Dkt. Julius Mwanandota, Daktari Mtafiti wa Mifugo. Huduma hizo ni pamoja na uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji na matumizi sahihi ya chanjo za mifugo, uchunguzi wa ubora na usalama wa vyakula vya mifugo, usajili na uhakiki wa viuatilifu vya mifugo, pamoja na utoaji wa ushauri wa kitaalamu kuhusu afya na kinga ya mifugo.


Baada ya kupokea maelezo hayo, Prof. Sheikh ameeleza kuridhishwa na maandalizi yaliyofanywa na TVLA, akiwapongeza wataalamu wa Wakala kwa namna wanavyoendelea kutoa elimu kwa wadau wa mifugo kuhusu huduma mbalimbali zinazolenga kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza tija ya uzalishaji na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.
