Back to top

"WANALAGHAI VIJANA KUHUJUMU MATAIFA YAO"

13 July 2026
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa baadhi ya Mataifa makubwa duniani hayafurahishwi na kasi ya maendeleo ya Nchi zinazoendelea, huku wakiwalaghai Vijana kuhujumu Mataifa yao.

Rais Samia ameyasema hayo Julai 13, 2026, wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali pamoja na Wakuu wa Sheria uliofanyika Jijini Arusha.

Amesema katika mazingira ya sasa ya ushindani wa Kimataifa, baadhi ya Vijana wamekuwa wakishawishiwa na kulaghaiwa ‘Kumezeshwa Sumu’ kuichukia Nchi yao pamoja na kuhujumu juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali zao.

“Nimemsikia mmoja wa Viongozi wakubwa duniani akisema kuwa yeyote anayewazidi kwa kasi ya maendeleo ni adui yao, Nchi zetu zinapopiga hatua mbele, wengine wanatafuta njia na mbinu za kuzivuta nyuma,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa dunia inaendelea kushuhudia Mataifa yakihujumiana kwa njia mbalimbali, huku baadhi ya Vijana wakipewa taarifa na mitazamo inayowafanya kuhujumu Mataifa yao wenyewe.

“Tunashuhudia Vijana wakilaghaiwa, wengine wakimezeshwa sumu dhidi ya Mataifa yao na kushawishiwa kuhujumu uchumi unaojengwa kwa nguvu kubwa,” amesema.