Back to top

MAPATO YA AIRTEL AFRICA YAFIKIA DOLA BIL.1.85

24 July 2026
Share

Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Africa imeanza mwaka wake mpya wa fedha wa 2026/27 kwa mafanikio makubwa, baada ya kuongeza mapato kwa asilimia 31 katika robo ya kwanza ya mwaka 2026/27, yakichochewa na kasi kubwa ya matumizi ya intaneti na huduma za kifedha kwa njia ya mtandao.

Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, Bw. Sunil Taldar, amesema mapato ya kampuni hiyo inayofanya kazi katika nchi 14 barani Afrika, ikiwemo Tanzania, yalifikia dola bilioni 1.853 za Marekani kwa robo mwaka iliyoishia Juni 30, 2026, ikilinganishwa na dola bilioni 1.415 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Faida baada ya kodi ilipaa kwa asilimia 27 na kufikia dola milioni 198. Kwa kuzingatia viwango vya fedha visivyobadilika (constant currency), mapato ya kampuni yalikua kwa asilimia 21.1, yakionyesha ukuaji thabiti katika huduma za sauti, intaneti na Airtel Money.

Ripoti hiyo inaonyesha ukuaji mkubwa katika maeneo yote makuu ya kibiashara ambapo soko la Nigeria liliongoza kwa kukua kwa asilimia 29.8, likifuatiwa na ukanda wa Afrika ya Kati na Magharibi inayozungumza Kifaransa (Francophone Africa) uliokua kwa asilimia 18, huku ukanda wa Afrika Mashariki ukikua kwa asilimia 17.8.

Ukuaji huo unachochewa na ongezeko kubwa la wateja ambapo katika nchi zote 14, jumla ya wateja wa Airtel iliongezeka kwa asilimia 11.6 hadi kufikia milioni 189, na asilimia 51 ya wateja wote wa kampuni hiyo sasa wanatumia simu janja (smartphones). 

Hali hiyo imesababisha idadi ya wateja wa intaneti kuongezeka kwa asilimia 15.5 hadi kufikia milioni 87.3.