
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amekosoa utamaduni wa kudai mahari kubwa, akisema tabia hiyo inawakatisha tamaa vijana wengi kuingia kwenye ndoa kutokana na gharama kubwa zinazowakabili.
Akizungumza kwenye sherehe ya harusi wilayani Kiruhura, Museveni amewataka wazazi kuacha kuwachukulia mabinti zao kama njia ya kujipatia utajiri kupitia mahari.
"Ninyi Wabanyankole mnaharibu kweli ukuaji wa jamii, wazazi kwa nini mnawauza watoto wenu? Ng'ombe 16, sijui ni ng'ombe wangapi, kwa nini mnataka kujipatia utajiri kupitia watoto wenu? kwa nini msifanye kazi na kujitafutia wenyewe?"Amesema Museveni.
Ameeleza kuwa kudai idadi kubwa ya ng'ombe na malipo mengine ya gharama kubwa kama mahari kunawafanya vijana wengi kushindwa kumudu gharama za ndoa, jambo linalochelewesha uanzishwaji wa familia na kuhimiza familia kupunguza matarajio ya mahari ili kurahisisha vijana kufunga ndoa, kuimarisha taasisi ya familia na kuchochea maendeleo ya jamii.
