Back to top

Vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Malaria mkoani Mwanza vyapungua.

26 April 2018
Share

Halmashauri za wilaya ya Ukerewe na Buchosa mkoani Mwanza bado zinaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Malaria, kutokana na wilaya hizo kuwa kandokando ya ziwa Victoria, huku vifo vitokanavyo na ugonjwa huo katika halmashauri zote nane za mkoa huo vikipungua kwa zaidi ya nusu kutoka 543 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 254 mwaka jana 2017.

Kaimu Mganga mkuu wa mkoa wa mwanza Dkt. Silas Wambura, amesema utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria nchini Tanzania wa mwaka 2015/2016, unaonyesha kiwango cha maambukizi katika mkoa wa Mwanza bado kiko juu kwa asilimia 15.1, wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 14. 

Hata hivyo kiwango hicho kinaelezwa kwamba kimepungua kutoka asilimia 19.1 kutokana na utafiti wa viashiria vya ukimwi na Malaria uliofanyika mwaka 2011 – 2012.

Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Estomiah Chang'a, akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Malaria duniani yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Getruda Mongella mjini Nansio, amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani ukerewe kusimamia matumizi sahihi ya vyandarua, ambavyo serikali imevigawa kwa wanafunzi wa shule za msingi na kuhakikisha kila mtu anashiriki kuharibu mazalia ya mbu waenezao Malaria.

Hadi sasa mazalia 468 yenye viluwiluwi vya mbu yametambuliwa na kati ya hayo 266 yameshapuliziwa dawa ya kuviangamiza.

Kwa upande wake, afisa mradi wa USAID boresha afya katika mikoa ya kanda ya ziwa na Magharibi Emmanuel Lesilwa anasema mikoa ya Kigoma, Kagera na Mwanza bado ina changamoto ya wagonjwa wengi wa malaria hivyo wao kama wadau wa afya wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.