
Operesheneni ya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa wanne katika hospitali ya Taifa Muhimumbili jijini Dar es Salaam umefanyika kwa mafanikio makubwa baada ya wagonjwa wawili kuruhusiwa siku ya leo kurudi nyumbani baada ya kupona kabisa huku madaktari walioshiriki katika zoezi hilo wakisema hayo ni mafanikio makubwa katika kuokoa maisha ya Watanzania wengi wanaosumbuliwa na figo kwa kutibiwa hapa nchini kwa sasa.
Mmoja wa madakatari Bingwa wa figo aliyeshiriki katika operesheni hiyo ya kupandikiza figo Dokta Onesmo Kisanga ameiambia ITV kuwa zoezi hilo limefanyika kwa mafanikio makubwa na kutoa fursa ya kuongeza huduma ya upandikizi wa figo baada ya serikali kuridhia kujengwa kwa jengo maalumu kupandikiza figo ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaosumbuliwa na figo.
Nao wagonjwa waliopandikizwa figo na sasa wamepona wameelezea furaha yao kwa Watanzania kwa huduma hiyo kupatikana hapa nchini huku waliojitolea figo wakiowaomba watanzania kuwa na moyo wa kusaidia wagonjwa pale wanapoona wanastahili kufanya hivyo.