
Serikali imesema mfumo wa vyama vingi nchini umesababisha kushuka kwa uzalendo kwa wananchi kutokana na baadhi ya wanasiasa kushabikia mitazamo na kampeni hasi dhidi ya serikali iliyopo madarakani.
Akijibu swali la Mbunge wa Kiwani Mhe.Abdalah Ali aliyeuliza baada ya miongo miwili na nusu faida gani imetapatikana za mfumo na vyama vya vingi na changamoto zilizojitokeza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,kazi,vijana,ajira Mhe Anthony Mavunde amesema mfumo huo umesababisha kuibuka kwa makundi ndani ya baadhi ya vyama vya siasa ambapo viongozi wamekuwa hawafanyi siasa za kistaarabu na kuchochea vurugu katika jamii.
Aidha amesema mfumo huo umeongeza gharama za kuendesha chaguzi za kisiasa katika ngazi mbalimbali pamoja na gharama za ruzuku ya serikali kwa vyama vingi vya siasa vyenye usajili wa kudumu na uwakilishi bungeni na katika ngazi ya serikali za mitaa.
Aidha amesema mfumo wa vyama vingi umewezesha kupanuka kwa wigo wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi ambapo hadi sasa kuna vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.