Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wamejenga zahanati katika vijiji 33 kwa nguvu zao ili kupunguza adha ya kusafiri umbali mrefu wa kutafuta huduma za matibabu.
Kwa upande wa serikali imesaidia kununua vifaa vya viwandani kukamilisha zahanati hizo.
Wananchi hao wamesema wameamua kujenga zahanati baada ya kuchoshwa na adha ya muda mrefu ya kutafuta huduma za matibabu mbali hali inayosababisha vifo vya wajawazito na watoto vijijini.
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bwana BRUNO MAPUNDA amesema wameguswa na jitihada za wananchi na kuamua kuagiza vifaa kutoka viwandani kwa bei nafuu ili kukamilisha zahanati zilizojengwa na wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Bwana GOMBO SAMANDITO GOMBO amesea kwa kushirikiana na wananchi ni azma yake kujenga zahanati katika vijiji vyote vya halmashauri hiyo ili kutimiza mpango wa serikali wa kila kijiji kuwa na zahanati.