
Wizara ya kilimo na umwagiliaji imeombwa kuweka kipaumbele cha kukabiliana na ndege waharibifu aina ya Kweleakwelea wanaoshambulia zao la Mtama aina ya Baraka na Masia mbegu ambayo imeonyesha kufanya vizuri katika mikoa ya kusini na kanda ya kati ikiwemo mkoa wa Dodoma na hivyo kurudisha nyuma juhudi za wakulima katika kupanda mazao yanayostaimili ukame.
Akizungumza na ITV iliyotembelea mikoa ya Lindi na Dodoma afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Bahi Jovin Barabata amesema ndege aina ya Kweleakwelea ni tatizo kubwa katika wilaya yake licha ya wizara ya kilimo na umwagiliaji kukabiliana nao.
Kwa upande wao baadhi ya wakulima wanaolima zao hilo kutoka mikoa ya Lindi na Dodoma wanasema licha ya mbegu hizo kufanya vizuri mashambani ndege waharibifu ni tatizo lakini pia masoko ni shida na hivyo baadhi yao kutumia kulisha mifugo.
Mbegu za mtama aina ya Baraka na Masia zimegunduliwa na taasisi ya utafiti wa kilimo Naliendele na zimeonyesha kufanya vizuri hasa katika maeneo yenye ukame.