Back to top

SERIKALI KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA DHARURA

13 July 2025
Share

Serikali kupitia Wizara ya Afya imesema imepunguza vifo vitokanavyo na dharura kwa kuweka miundo mbinu ya vituo vya dharura kwa zaidi ya asilimia 40 kwa Watanzania.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo  wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri, Jijini Dodoma unaoenda na kauli mbiu 'Wajibu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika Kuimarisha Ubora wa Huduma za Afya kuelekea Bima ya Afya kwa Wote'.

Amesema katika kuhakikisha vifo hivyo vinaendelea kupungua Wizara ya afya kwa kushirikiana na mfuko maalum wa magonjwa ya mlipuko umeingia makubaliano kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 kuimarisha huduma za dharura katika maeneo yote nchini.

Aidha, Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali kupita Wizara ya Afya inatarajia kuanzisha televisheni ya Afya (Afya TV) kwa lengo la kutoa taarifa na elimu ya afya kwa wananchi ili  kujikinga na magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mlipuko. 

Waziri Mhagama meeleza kuwa Tanzania imevunja rekodi ya kuwa kati ya nchi mbili hadi tatu ukanda wa Afrika Mashiriki zenye mashine inayofuatilia uchunguzi na matibabu ya saratani inayogharimu zaidi ya  Shilingi Bilioni 18.

"Pia sisi ni kati ya nchi tatu (3) katika ukanda wa SADC tuliyokuwa na hiyo mashine ya PET-Scan, Tanzania, nchi ya sita (6) ukanda  wa SADC tulio na mashine nyingi za MRI haya ni matunda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa upande wa Tiba Utalii  tumeongeza  idadi ya watalii 12000 kwa kipindi kifupi wameingia kwenye nchi yetu kwa ajili ya matibabu" Ameeleza

Amewashukuru watumishi wote wa sekta ya afya wakiongozwa na madaktari viongozi kwa kuhakikisha huduma bora za afya zinaendelea kutolewa kwenye hospitali na vituo vyote vya afya nchini