
Kocha wa klabu ya Newcastle United Steve Bruce ameweka wazi kuwa alipokea ushauri kutoka kwa kocha wa zamani wa klabu ya Manchester United Sir Alex Ferguson kabla ya kuingia uwanjani kuvaana na Manchester United na kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya timu hiyo katika maisha yake ya ukocha.
Bruce aliamua kumchezesha Matty Longstaff kwa mara ya kwanza katika ligi ya England sambamba na kaka yake Sean ambaye anawindwa na klabu ya Manchester United.
Maamuzi yake yalionekana yenye busara na mafanikio kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 kufunga bao la pekee na la ushindi dhidi ya Manchester United jumapili iliyopita.
Matokeo hayo yamewaacha United wakiwa na pointi 2 tu juu ya timu zinazotarajia kushuka daraja msimu huu kwenye msimamo wa ligi ya England wakiwa hawajashinda katika michezo mitatu ukiwa ni mwanzo mbaya tangu msimu wa mwaka 1989.
Bruce ambaye ni mchezaji wa zamani wa Manchester United ameweka wazi siri ya kuifunga Manchester United siku hiyo ni kwamba "nilifanya mazungumzo na Sir Alex Ferguson Ferguson ajili ya ushauri kabla ya mechi hiyo. Na mara nyingi nampigia Sir Alex kwa ushauri mdogo nafanya sasa na hata baadae na nimeshazungumza naye mara kadhaa" alisema Steve Bruce.
"Amekuwa akinishauri katika Muda ninaohitaji ushauri mara nyingi amekuwa akifanya hivyo. Na nilimuona jumatatu usiku kwenye uwanja wa Old Trafford lakini hupaswi kujua nini aliniambia". Aliongeza Steve Bruce.