Hekta elfu mbili katika Hifadhi ya msitu wa mlima Matogoro uliopo wilayani Songea mkoani Ruvuma zimeteketea kwa moto na kuathiri vyanzo vya maji vilivyoko katika msitu huo.
Afisa wa wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Songea Juma Mbwambo anasema kuwa msitu huo umechomwa na watu wanaoandaa mashamba na wachoma mkaa ambao wakati maofisa wa TFS wakihangaika na kuzima moto wao wanapata nafasi ya kubeba mkaa msituni.
Mhandisi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea (SOUWASA) John Kapinga anasema kuwa upatikanaji wa maji manispaa ya Songea umepungua kutokana na uharibifu wa mazingira kwa kuwa katika msitu huo kuna vyanzo nane vya maji vilivyoathirika kikiwemo chanzo cha mto Ruvuma.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Songea Bw.Pololet Kamando Mgema amewataka wananchi kujiona sehemu ya misitu na kuilinda na kwamba watakaobainika kuhusika na uhalifu huo watachukuliwa hatua.