Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Kitengo cha Rufaa imeanza hatua za awali za kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na serikali kupinga ushindi wa wadau wa sekta ya habari waliokuwa wanalalamikia kukandamizwa kwa uhuru wa habari kwenye kesi namba tano ya mwaka 2019.
Katika kesi hiyo namba tano ya mwaka 2019 wawakilishi wa walalamikaji ambao ni Baraza la Habari Tanzania MCT, kituo cha sheria na haki za binadamu ,na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania walishinda baada ya mahakama ya Jumuiya ya Afika mashariki kutoa mamuzi yaliyoonyesha kuwa hoja za upande wa walalamikaji zilikuwa na msingi jambo lililopelekea upande wa walalamikiwa ambao ni serikali kuonyesha nia ya kukata rufaa.
Hata hivyo baada ya serikali kukata rufaa hiyo upande wapili wa wadau wa habari waliwasilisha pingamizi ya rufaa hiyo kwa madai kuwa baadhi ya taratibu zimekiukwa ikiwemo ya kuwasilishwa nje ya muda unaotakiwa kisheria huku upande wa serikali nao wakidai kuwa wana sababu za msingi na zinazokubalika za kuchelewa kwa kuwasilisha rufaa hiyo.
Kufuatia mapingamizi hayo jopo la majaji watano wa mahakama hiyo Kitengo cha Rufaa wakiongozwa na Rais wa mahakama hiyo DK. Emanuel Ugirashibuje wamekutana na wanasheria wa pande zote mbili na kuweka makubaliano ya kuanza kusikiliza mapingamizi hayo .
Katika kikao hicho baadhi ya wanasheria wa wadau wa habari akiwemo Mpale Kaba Mpoki na Jebra Kambole wamesema wamekubaliana kila upande kuwasililsha hoja zake kwa maandishi ambapo upande wa wadau wa habari watawasilisha hoja zake tarehe 04/03/2020 na upande wa serikali watatakiwa kujibu tarehe 24/03/2020.