Wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na bodi ya filamu nchini imeandaa mkakati wa kutumia mfumo wa filamu kutangaza vivutio vilivyopo nchini zikiwemo hifadhi za taifa ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini.
Utekelezaji wa mkakati huo kwa mujibu wa katibu mkuu wa wizara ya maliasili na utalii Profesa Adolph Mkenda utayashirikisha makampuni makubwa ya filamu kutoka nje na kwamba nguvu kubwa itaelekezwa kwenye utangazaji wa hifadhi ambazo bado hazijatambulika zaidi kimataifa.
Ili kufanikisha mpango huo kaimu katibu mtendaji wa bodi ya filamu nchini Dkt.Kiagho Kilonzo anasema wameanza kuondoa urasimu wa upatikanaji wa vibali vya waandaaji wa filamu kuingia nchini
Mpango huo pia unawashirikisha wadau wengine wa sekta ya utalii nchini ambao wameahidi kuwekeza nguvu kuufanikisha.