
Serikali mkoani Geita imeifunga kwa wiki mbili shule ya sekondari Geita huku ikiwafukuza shule wanafunzi kumi na moja na walimu zaidi ya kumi wakihamishwa shuleni hapo kutokana na bweni la wavulana kuteketea moto usiku wa kuamikia leo na kujeruhi wanafunzi watatu hii ikiwa ni mara ya tatu kwa shule hiyo kuungua moto ndani ya mwezi mmoja hali iliyosababisha hofu na sintofahamu kwa wanafunzi na wazazi.
Hatua hiyo imechukuliwa na mkuu wa mkoa wa Geita Bi Rosemery Senyamule kutokana na matukio ya moto kutokea mara tatu ndani ya mwezi moja na kuteketeza maambara mbili,ghala la kuhifadhia kemikali za majaribio ,bweni la wavulana pamoja na darasa la kuhifadhia vifaa vya wanafunzi.
Mkuu huyo wa mkoa pia ameagiza kuondolewa kwa walinzi wote wa shule hiyo na kuletwa walinzi wengine wenye mafunzo ya kijeshi ili kuimarisha usalama katika shule hiyo.