Back to top

Mabalozi tangulizeni maslahi ya taifa - Waziri Mkuu.

03 October 2021
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amesema mabalozi wanaoteuliwa kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi wanapaswa kutanguliza maslahi ya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma wakati alipokutana na mabalozi saba watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Sweden, Rwanda, India, Ethiopia, Uswisi na Jamhuri ya Korea.

 
Mabalozi hao na nchi zao kwenye mabano ni Luteni Jenerali Yacoub Mohamed (Uturuki), Grace Olotu (Sweden), Meja Jenerali Richard Makanzo (Rwanda), Anisa Mbega (India), Innocent Shiyo (Ethiopia), Hoyce Temu (Uswisi) na Togolani Mavura (Jamhuri ya Korea).

 
Waziri Mkuu amesema mabalozi hao wana jukumu la kukuza uchumi wa Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi na amewataka waangalie ni jinsi gani wanaweza kuinua sekta nyingine kama vile utalii kwa kuitangaza Tanzania huko waendako ili kuvutia watalii wengi zaidi. 

Kuhusu wana-diaspora, Waziri Mkuu amewataka mabalozi hao wawatambue walioko huko waendako, watambue biashara na kazi zao na wawashawishi wafungue matawi ya kampuni zao huku kwao. Amewataka wasiache kuwapa taarifa za mara kwa mara juu ya mambo yanayofanyika hapa nchini.