Back to top

UJENZI WA NANGANGA RUANGWA UENDANE NA THAMANI YA FEDHA.

26 January 2022
Share

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof.Makame Mbarawa amemtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi kuhakikisha wananchi wanaelimishwa ili kupisha eneo la mradi ujenzi wa barabara kutoka Ruangwa mjini hadi Nanganga ili kumuwezesha Mkandarasi kufanya kazi, na wananchi wenye malalamiko yapatiwe ufumbuzi kwa haraka.
.
Ametoa kauli hiyo alipotembelea ujenzi wa barabara kutoka Ruangwa mjini hadi Nanganga yenye urefu wa Kilometa 53.2 ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi wa kumi na moja mwaka 2022.

Waziri Mbarawa pia amemtaka Msimamizi kampuni ya TECU kuhakikisha anazingatia viwango vilivyokubaliwa katika mkataba ili kuwezesha barabara kudumu kwa muda mrefu na kuchochea maendeleo ya wakazi wa mkoa wa Lindi.

Aidha Prof.Mbarawa amesema zaidi ya shilingi bilioni 59 zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo sehemu ya Nanganga/Ruangwa hivyo kumtaka Msimamizi wa ujenzi huo kampuni ya TECU na wafanyakazi wa TANROADS mkoa wa Lindi kuhakikisha ujenzi wake unaendana na thamani ya fedha na kuharakisha usanifu wa kina kwa haraka sehemu iiliyobaki ya Nachingwea/Ruangwa KM 52.8.