
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefanya uteuzi wa madiwani watano wa viti maalum (Chama cha Mapinduzi) baada ya waliokuwepo awali kufariki na mwingine kupoteza sifa.
Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 28, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi Gerald Mwanilwa, imesema kuwa madiwani hao wameteuliwa kujaza nafasi kwa Mujibu wa kifungu cha 86A cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa NEC imefanya uteuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Dhamana ya Serikali za mitaa, ambaye kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13,(1)(a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wa nafasi za wazi za madiwani wanawake wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya walioteuliwa awali kufariki dunia na mwingine kupoteza sifa.
Aidha Madiwani walioteuliwa ni Cintya Felix Mwalunde (Halmashauri ya wilaya ya Songwe), Amina Alli Kea (Halmashauri ya wilaya ya Muheza), Theresia Peter Mushi (Halmashauri ya wilaya ya Moshi), Leah Constantin Mbilinyi (Halmashauri ya wilaya ya Ludewa) na Amina Ramadhani Mweri (Halmashauri ya wilaya ya Singida).
