Back to top

Sumu kuvu yatishia usugu wa dawa kwa mifugo, binadamu.

14 February 2022
Share

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) umesema katika mwaka ujao wa fedha 2022/2023 unatarajia kuongeza wigo wa kufanya vipimo vya ubora wa vyakula vya mifugo ili kubaini aina za sumu kuvu ambazo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa binadamu na mifugo.

Mtendaji Mkuu wa TVLA Dkt. Stella Bitanyi amebainisha hayo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa zoezi la kuhakiki ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa hapa nchini lililofanyika mwishoni mwa wiki, zoezi ambalo limefanywa katika wilaya za Temeke na Ubungo na wataalamu kutoka TVLA.

Dkt. Bitanyi amesema Wakala  huo unatarajia pia kupima mabaki ya ‘antibiotic’ na dawa nyingine za mifugo ndani ya vyakula vya mifugo ili kuhakikisha ubora wa vyakula vya mifugo kwa kutokuwa na mabaki ya dawa ambazo zinaweza kusababisha usugu wa dawa kwa mifugo pamoja na binadamu atakayetumia mazao yanayotokana na mifugo hiyo.

Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu huyo wa TVLA ametoa wito kwa wazalishaji wa vyakula vya mifugo nchini pamoja na wafugaji kuhakikisha wanafikisha sampuli za vyakula katika maabara hiyo ili kupima ubora wa chakula ambacho kinastahili kutumiwa na mifugo pamoja na malighafi ambazo zitatumiwa katika kutengeneza vyakula hivyo.

Amebainisha kuwa matumizi ya vyakula sahihi vya mifugo ambavyo vina virutubisho vinavyostahili, vitamuwezesha mfugaji kufuga kwa tija kwa kuwa mifugo itakuwa katika muda unaotakiwa kitaalamu na kufikia kiwango cha uzito unaotakiwa sokoni.

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo upo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi umekuwa ukifanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo ili vyakula hivyo viwe katika viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi ya mifugo na kuleta tija kwa mfugaji.