Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, ameushukuru Mfuko wa nchi zinazozozalisha Mafuta kwa wingi Duniani (OPEC FUND), kwa kuwekeza hapa nchini zaidi ya dola za Marekani milioni 218, sawa na shilingi za Tanzania, bilioni 504, kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Nchemba, alitoa shukrani hizo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika hilo ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh, ambapo walijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Mfuko huo.
Alisema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali, ukiwemo mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe, mradi wa barabara ya Kazilambwa-Chagu, barabara ya Uvinza-Ilunde – Malagarasi pamoja na kufadhili mradi wa kupambana na Umasikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua umuhimu wa Sekta Binafsi katika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi na imejitahidi kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyajibiashara katika sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa OPEC FUND, Dkt. Alkhalifa Abdulhamid Saleh, aliahidi kuwa Mfuko wake utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.
Alisema kuwa Mfuko huo umepanga pia kushirikiana na Tanzania kuisaidia sekta binafsi ili iweze kukua zaidi na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa sekta binafsi ndiyo injini ya ukuaji huo wa uchumi na maisha ya wananchi.
