Back to top

Waziri Nchemba atoa rai kwa wadau sekta ya mifugo.

04 April 2022
Share

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa rai kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini kuisadia serikali kutimiza nia yake ya kuimarisha uzalishaji wa nyama na maziwa ili kuongeza tija na kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo jijini Dodoma, alipokutana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, wataalam kutoka Wizara hiyo na Wizara ya Fedha na Mipango, pamoja na Wazalishaji binafsi katika sekta za maziwa na nyama nchini.

Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa sekta ya mifugo itakuwa na mchango mkubwa katika kukuza kipato cha wananchi hususani vijana lakini pia itaongeza mapato ya nchi kwa kuzalisha bidhaa za nyama na maziwa zitakazo uzwa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aliwataka wadau hao kuwa walimu wa kuwaongoza na kuwafundisha vijana namna ya kuzalisha mifugo bora kwa ajili ya nyama na maziwa na kwa kuwa wana mtandao wa masoko, ni rahisi kwa wafugaji kupata maeneo ya kuuza mazao yao.