
Tanzania na Kenya zimetia saini makubaliano ya Mpango Kazi wa kuendelea na kazi ya Uimarishaji Mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizo kutoka eneo la Ziwa Natron hadi Namanga mkoani Arusha.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu wa Mipaka kati ya nchi hizo kilichokuwa na lengo la kupokea mawasilisho ya utekekezaji kazi za awamu ya kwanza na kuangalia namna bora ya kukamilisha awamu ya pili.
Utiaji saini ulifanyika Wilayani Tarime mkoa wa Mara kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor na Bi.Juster Nkoroi ambaye ni Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO).



Awamu ya kwanza ya uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo ulikuwa wa kipande cha urefu wa Km 238 kuanzia Ziwa Victoria hadi Natron ambapo awamu hiyo ilikamilishwa hivi karibuni kwa kipande cha Km 23 kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara hadi Ziwa Natron.
Katika makubaliano ya Mpango Kazi, utekelezaji Uimarishajji Mpaka wa Tanzania na Kenya awamu ya pili utaanza mwishoni mwa mwezi April 2022 na kutarajiwa kukamilika Juni 2022 kwa kipande cha Km 110 kutoka Ziwa Natron Hadi Namanga mkoani Arusha kufanyiwa kazi.
