
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amemsimamisha kazi mtendaji wa kata ya Kwenjugo kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa zahanati ya Bwila pamoja na kuwafunga pingu wananchi waliokuwa wakihoji matumizi ya fedha za ujenzi wa zahanati.
Hatua ya mkuu wa Wilaya inakuja siku moja baada ya Waziri wa TAMISEMI, Mhe.Inocent Bashungwa kumuagiza kufika kwenye Zahanati ya Bwila na kufanya uchunguzi wa tuhuma za Mtendaji wa Kata ya Kwenjugo zinazomkabili, baada ya taarifa yake kuripotiwa hapa ITV na kupongeza kituo hiki kuibua taarifa hiyo.

Aprili 17, 2022 ITV iliripoti kuwepo mvutano mkali kati ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Handeni mkoani Tanga na Mtendaji wake wa kata ya Kwenjugo baada ya Mwenyekiti huyo kufika kwenye ujenzi wa Zahanati ya Bwila na kuhitaji taarifa ya ujenzi huo uliogharimu zaidi ya shilingi Milioni 50.
Aidha maelekezo ya bashungwa aliyoyatoa Aprili 18 kutokana na mvutano uliokuwepo kufuatia tuhuma za Mtendaji wa Kata ya Kwenjugo kwa kumshawishi Mwenyekiti wa Mtaa akubali kula njama ya kuiba fedha za ujenzi wa zahanati alisema.
"Nawashukuru ITV kwa taarifa hii ya tuhuma za Mtendaji wa Kata ya Kwenjugo, Halmashauri ya Handeni Mji kujaribu kumshawishi Mwenyekiti wa Mtaa akubali kuweka 'cha juu' kwenye gharama za vifaa vya ujenzi wa zahanati, matendo haya hayavumiliki hata kidogo"-Alisema Bashungwa.ndipo akaagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya Mtendaji wa Kata iwapo itathibitika amekosa uaminifu katika utumishi wa Umma.
