Back to top

Nchemba aishukuru Benki ya Dunia kwa kuahidi kuisaidia Tanzania

19 April 2022
Share

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na madhara ya UVIKO-19 na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine.

Dkt. Nchemba amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoendelea Jijini Washington DC, Marekani.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wataalam wa Benki ya Dunia, IMF na Benki ya Maendeleo ya Afrika, watakutana ili kupitia maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili utekelezaji wa miradi hiyo ianze mwaka mpya wa fedha 2022/2023.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, alipongeza mabadiliko makubwa ya kisera na kiuchumi yanayoendelea nchini Tanzania, ambayo anaamini yatasaidia kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.