Back to top

Tanzania kunufaika na misaada ya IMF na Benki ya Dunia

24 April 2022
Share
Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Tanzania inatarajia kunufaika zaidi na fursa za mikopo na misaada inayotolewa na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF baada ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara katika Taasisi hizo na kufanya mazungumzo na uongozi wake wa juu, Jijini Washington DC, nchini arekani.
 
Dkt. Nchemba alieleza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine, amekutana na kujadiliana masuala kadhaa kuhusu Tanzania na Rais wa Benki ya Dunia Bw. David Malpass na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa Bi. Kristalina Georgiva, ambapo viongozi hao wamemwahidi kumsaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
 
Alieleza kuwa katika mazungumzo yao, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alieleza kuhusu hatua kubwa za maendeleo ambazo Tanzania imepiga katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kuziomba taasisi hizo kutazama kwa upana athari za kiuchumi ambazo nchi nyingi zinapitia kutokana na madhara ya uviko 19 na vita baina ya Urusi na Ukraine na kuzisaidia.
 
Dkt. Nchemba alisema kuwa Mheshimiwa Rais Samia aliziomba taasisi hizo za fedha kuiongezea fedha nchi yake na kuiwezesha kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa zikiwemo ngano, mafuta ya kula, mbolea na bidhaa nyingine ili kuwapunguzia makali ya maisha wananchi wake kupitia miradi ya kuendeleza kilimo bora na chenye tija.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, alieleza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pia amewasilisha maombi kwenye taasisi hizo kusaidia utekelezaji wa miradi itakayosaidia kukuza ajira kwa vijana.
 
Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anaongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, inayofanyika Jijini Washington DC, Marekani.