
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Malawi Balozi Humphrey Polepole na kumsihi Balozi Polepole kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zinazopelekwa katika kuendesha ubalozi huo ili kuongeza tija ya uwakilishi nchini humo.
Aidha amemuasa kuwaunganisha watanzania wanaoishi nchini Malawi ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amemtaka Balozi Polepole kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.
