Back to top

Majaliwa:Taasisi za umma tumieni mfumo wa TANePS.

06 May 2022
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha kuwa taasisi zote za umma zinatumia Mfumo wa Ununuzi kwa Njia ya Mtandao (TANePS) na hatua kali zichukuliwe dhidi ya maafisa masuuli ambao taasisi zao zitakaidi matumizi ya mifumo katika ununuzi wa umma.

Maagizo hayo aliyatoa jijini Arusha, wakati akifungua kongamano la Wiki ya ununuzi wa Umma lililowakutanisha wadau wa ununuzi takribani 1000 wakiwemo maafisa ugavi, wazabuni, wajumbe wa bodi na maafisa masuuli kutoka Wizara, taasisi, Halmashauri na sekta binafsi.

Akizungumza katika kongamano hilo Mhe. Majaliwa alisisitiza matumizi ya mifumo katika ununuzi wa umma pamoja na kuhakikisha ufanisi wa mifumo hiyo ili huduma zipatikane kwa wakati ukiwemo umakini wa wanaosimamia mifumo na kuwa na njia mbadala ikitokea changamoto ya mtandao.

Pia Mhe. Majaliwa aliiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kupitia kitengo chake cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa za Kifedha na GPSA ihakikishe bei zote za bidhaa na huduma zinazotumika sokoni kwa jumla na rejareja zinaingizwa kwenye mfumo wa TANEPS na kuwa na kiwango cha ukomo wa bei zitakazotumika Serikalini.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya ununuzi wa umma kwa maslahi ya Taifa kwa kufanya maboresho katika Sheria ya ununuzi wa umma.