Back to top

MABULA AAGIZA KUKAMILIKA UTHAMINI WA FIDIA MGODI WA NYANZAGA

10 June 2022
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula amemuagiza Mthamini Mkuu wa Serikali, Evelyne Mugasha kukamilisha uthaminishaji fidia kwenye eneo la mradi wa mgodi wa Nyanzaga uliopo Sengerema mkoani Mwanza baada ya wananchi wa eneo hilo kuelewa taratibu za fidia kwenye eneo hilo.

Mgodi wa Nyazaga unaoendeshwa kwa njia ya ubia kati ya kampuni ya OreCorp Tanzania Limited (84%) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (16%) upo kata ya Ngoma kwenye vijiji vya Sota na Nyabila na kufunguliwa kwake kunaenda sambamba na zoezi la utwaaji ardhi kwa eneo lote lililoidhinishwa katika leseni ya uchimbaji madini.

Changamoto katika Programu ya kuwahamisha watu na makazi katika eneo la mgodi wa Nyanzaga lenye ukubwa wa ekari 5,683 ni baadhi ya wananchi wachache kutoridhika na kiasi cha kiwango kilichoidhinishwa kutumika katika malipo ya fidia ya ardhi na uwepo wananchi wanaodai kuwa na haki ya umiliki maeneo ya milima.

Hata hivyo, tayari wananchi 1,236 sawa na asilimia 85 wamechukua form namba tatu kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kulipwa fidia kupisha program ya kuanza kwa mradi wa mgodi wa Nyanzaga na wananchi 216 sawa na asilimia 15 bado hawajachukua form hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula aliyekwenda kutoa ufafanuzi wa fidia kwa watu wanaotakiwa kuhamishwa katika eneo la mgodi huo, kwa wale wananchi waliokubali kuchukua fomu namba tatu taratibu za kuthaminishwa zikamilishwa haraka ili waweze kulipwa fidia na wale wasiokuwa tayari taratibu za uthamini ziendelee mpaka watakaporidhika.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Sota katika kata ya Igalula wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakati wa kufuatilia zoezi la kuwahamisha watu na makazi kwenye mgodi wa Nyazaga Juni 9, 2022, Dkt Mabula amesema uamuzi wa serikali katika kulipa fidia ya kuwahamisha wananchi wa eneo hilo umezingatia taratibu zote za kisheria zikiwemo za kimataifa na hakuna mtu atakayepunjwa au kukopwa.