
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro amesema Jeshi la Polisi litaendeleza ushirikiano na Jeshi la Polisi nchini Malawi pamoja na kuendelea kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu pamoja na kufanya operesheni za pamoja kwa lengo la kuhakikisha nchi hizo zinakuwa salama.
IGP Sirro amesema hayo alipokutana na mgeni wake Dakta.George Inja ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Malawi ambapo amesema kuwa kutokana na ushirikiano huo kutarahisisha kukamatwa kwa wahalifu wanaofanya uhalifu nchi moja na kutorokea nchi nyingine.
Kuhusu wahamiaji haramu IGP Sirro amesema, wataendelea kuzishirikisha nchi nyingine katika kukabiliana na matatizo ya uingiaji wa wahamiaji haramu.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Malawi, Dakta.George Inja amesema Tanzania na Malawi zimeendelea kuwa na ushirikiano mkubwa na kwamba nchi hizo zimekuwa na matukio ya uhalifu unaofanana ikiwemo wizi wa magari unaofanyika kwenye nchi hizo na kuuzwa nchi nyingine, amemhakikishia IGP Sirro kuwa wataendelea kufanya operesheni za pamoja kwenye mipaka ili kudhibiti matukio ya namna hiyo.
