
Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan ameridhia kusamehewa riba ya kodi ya pango la ardhi kwa wadaiwa sugu kwa masharti kwamba wadaiwa hao wawe wamelipa madeni ya msingi ndani ya miezi sita kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2022.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula katika mkutano na wananchi wa kijiji cha Nyachoka wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa zoezi la kukabidhi hati miliki za kimila.


Dkt.Mabula amesema yeye pamoja na Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusamehe watakutana na kupanga namna bora ya kutekeleza msamaha huo.
"Najua kuna wengi wanadaiwa madeni ya muda mrefu kwa hiyo kumetokea msamaha kuanzia mwezi julai mpaka desemba mwaka huu, watakaoweza kulipa ndani ya miezi hii sita, wale ambao madeni yao yana miaka mitano kurudi nyuma watalipa bila ile tozo ya riba"Alisema Dkt. Mabula.


