Back to top

RAIS SAMIA ASEMA WATANZANIA WOTE NI MASHUJAA

25 July 2022
Share

Rais wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania wote ni mashujaa kwa kuwa ushujaa siyo kupambana katika vita vya ukombozi pekee, bali ni pamoja na kuhakikisha nchi inakuwa na amani, huduma bora za afya, maji, elimu ustawi na usalama wa wananchi.

Ametoa kauli hiyo katika kilele cha Kumbukumbu ya Mashujaa yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma ambako amependekeza Ofisi ya Waziri Mkuu itafute eneo kubwa lenye uwezo wa kujengwa mnara mkubwa  wa mashujaa kwa heshima ya makao makuu ya nchi.

Rais amesisitiza dhamira ya serikali ya kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma na kwamba mipango yote ya ujenzi wa mji wa serikali Mtumba, uimarishaji wa miundombinu na mipango ya maendeleo ya makao makuu ya nchi inaendelea na hakuna kurudi nyuma.

Amewataka Watanzania waendelee kuenzi michango ya mashujaa wa taifa, Baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume, kwa kuweka misingi imara ya utaifa amani, utulivu na mshikamano unaolipa taifa heshima pote duniani.

Sherehe hizo za mashujaa ambazo pia zimehudhuriwa na Marais wastaafu mzee Ali Hassan Mwinyi na Dkt.Jakaya Kikwete, pia zimehudhuriwa na viongozi wa serikali waliopo na wastaafu pamoja na wawakilishi wa waliopigana vita vya ukombozi na viongozi wa dini madhehebu mbalimbali wameomba dua.

Katika sherehe hizo Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mkuki na ngao kwenye Mnara wa Mashujaa, Mkuu wa Majeshi Jenerali Jacob Mkunda ameweka sime, mwakilishi wa Mabalozi ameweka shada la maua, mzee Omari Mhando Shangali aliyepigana vita ya Pilii vya Dunia ameweka shoka na Meya wa Jiji la Dodoma ameweka upinde na Mshale.