Back to top

MAWAZIRI PITIENI UPYA MIKATABA – MAJALIWA

13 August 2022
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wapitie upya mikataba ambayo nchi kupitia wizara zao zimeingia na nchi mbalimbali kwenye sekta zao ili kubaini maeneo ambayo yanahitaji kukamilishwa na kufanyiwa kazi.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ni muhimu Wizara zenye majadiliano ya mikataba na nchi nyingine zizingatie umuhimu wa majadiliano hayo na kutumia wataalamu wenye uzoefu kwenye maeneo hayo.

Ametoa kauli hiyo wakati akifunga kikao kazi cha Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu wao, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Amesisitiza kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, izingatie maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa Halmashauri zote nchini zinakuwa na makadirio stahiki katika malengo ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka ujao wa fedha sambamba na kuimarisha na kuibua vyanzo vipya vya mapato.

"Tusijivunie tu kukusanya asilimia mia moja wakati tumekadiria mapato kidogo na kuna fursa ya kukusanya zaidi, mabaraza ya madiwani na watendaji wetu wafanye mapitio ya maeneo yote ya makusanyo kuona eneo hilo kwa mwezi wanakusanya kiasi gani na kujiridhisha kama ndiyo mapato halisi yanayokusanywa.”Majaliwa 

Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ifanye uchambuzi wa Mpango wa kuikwamua Afrika Kiuchumi, hususani Tanzania na kuainisha fursa zilizopo na iweke mikakati ya kuzitumia.

"Suala hili lifanywe kwa haraka kwani mwelekeo wa Mheshimiwa Rais kwenye suala la uchumi hasa wa kilimo ni kuwachochea Watanzania kujikwamua kiuchumi. Tusipoteze fursa hii kama ina tija kwa nchi"Amesisitiza.

Kadhalika ameziagiza Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakutane na kujadili kwa pamoja mwingiliano wa kisheria kuhusu suala la uhakiki wa uthamini wa fidia wanazopaswa kulipwa wananchi baada ya Mthamini Mkuu wa Serikali kufanya uthamini wa maeneo yanayopaswa kulipwa fidia.