
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Mashimba Ndaki amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kushirikisha wadau wa sekta ya mifugo kupanga bei elekezi za kuuzia mifugo katika minada ili kuwawezesha wafugaji na wafanyabiashara kuuza mifugo yao kwa bei ambayo wao watakuwa wameshiriki kuipanga.
Ameeleza hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada wa Kimataifa wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita.
Amesema suala la kuwa na bei elekezi, Serikali inalifanyia kazi na tayari Wataalam walishaandaa na hatua iliyopo sasa ni ya kuwashirikisha wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ili kwa pamoja waweze kukubaliana na kuja na bei ambayo itakuwa imeridhiwa na pande zote.
Ameongeza kwa kusema kuwa sambamba na bei elekezi Serikali inataka sasa mifugo yote nchini ianze kupimwa kwa kilo kama ambavyo mifugo itapimwa kwa kilo katika mnada huo wa kisasa wa Buzirayombo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe.Medard Kalemani ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kujenga mnada huo wa Kimataifa Wilayani humo huku akiongeza kwa kuiomba kuhakikisha mradi huo unamalizika haraka ili wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine waanze kuona matunda yake.
