
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watendaji wote waliohusishwa na ubadhirifu wa mali za umma na uhujumu uchumi katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar (CAG) ya mwaka wa fedha 2020/2021.
Rais Mwinyi ameeleza hayo baada ya kupokea Ripoti ya Taarifa ya CAG katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais Dk.Mwinyi ameitaka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kujitathmini upya kiutendaji, pia Rais Dk.Mwinyi ameitaka Mamlaka hiyo kuifanyia kazi ripoti iliyowasilishwa yenye taarifa za upotevu wa fedha.
Amesema kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya kesi hizo watuhumiwa wamekiri kuhusika na matukio hayo na wengine kukubali kurejesha fedha serikalini, lakini hakuna hatua za kisheria zilizobainishwa kuchukuliwa.
Dk.Mwinyi ametolea mfano wa tukio la Wizi wa fedha lilitokea ZRB kupitia mfumo wa Mtandao, ambalo hadi sasa halijaainishwa hatua zilizochukuliwa na kusema utamaduni huo umefanya vitendo kama hivyo kujirejea mara kwa mara.
Amewataka Viongozi wote walioko serikalini kuona ukubwa wa tatizo hilo na kutaka hatua za msingi kuchukuliwa kwa wote waliohusika.
Katika hatua nyengine Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ilifanya uamuzi wa kuondoa jukumu la Wizara ya Afya kununua dawa na jukumu hilo kulikabidhi Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, lakini inashangaza Uongozi wa Hospitali hiyo nao unanunua dawa hizo kwa wauzaji wale wale waliokuwa wakichangia upotevu wa fedha nyingi za Serikali.
Ametumia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati CAG Dk.Othman Abass Ali kwa moyo wa kujitolea na kubainisha kasoro mbali mbali zilioko katika Wizara na taasisi za Serikali.
