Back to top

WIZARA YA AFYA YATOA TAHADHARI AJALI ZA BARABARANI.

22 December 2022
Share

Wizara ya Afya imewataka watumiaji wote wa vyombo vya moto barabarani, katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya krismasi, na mwaka mpya kuchukua tahadhari, ili kuepuka ajali zinazosababisha vifo, ulemavu wa kudumu na kuipa Serikali mzigo mkubwa wa kuhudumia wahanga.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi, alipofanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, na kutembelea wodi za wagonjwa wa upasuaji ambapo zaidi ya asilimia 70 ni wagonjwa wa ajali.

Amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani kuwapima madereva afya ya mwili na akili, ili wanaogundulika kuwa na tatizo waende hospitali kupata tiba stahiki na kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya moto, ili vile vitakavyobainika kuwa na hitilafu vizuiwe kutoa huduma kwani ajali zinapotokea kazi kubwa inahamia hospitalini.

Takwimu kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), zinaonesha kuwa katika kipindi cha Aprili hadi Juni, 2022 wagonjwa wa ajali walikua 1,917 na kipindi cha Julai hadi Septemba, 2022 wagonjwa wa ajali walikua 2,410, hivyo katika vipindi viwili hivyo asilimia 70 zilikua ajali za barabarani.