
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata majambazi sugu 4, kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya unyang’anyi wa kutumia silaha, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na mikoa ya jirani, huku likibainisha kuwa ukamataji huo ulitokana na taarifa fiche ya kuwepo kwa kundi hilo, la kihalifu, ambalo lilionekana kuanza kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha kuanzia Januari 01, 2023 hadi Januari 07, 2023.
.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ambapo alibanisha kuwa watuhumiwa hao ambao kwa sasa wapo katika hali mbaya baada ya kujeruhiwa na risasi, wakati wa majibizano ya risasi na polisi eneo la Mabibo External, walisalimisha silaha mbili ikiwemo bunduki aina ya AK 47, iliyokutwa na magazine yenye risasi 24 pamoja na bastola ndogo huku pia wakikutwa na pikipiki mbili pamoja na vifaa vingine mbavyo wanadaiwa kuvitumia kwenye uhalifu.
.
Aidha, kwa upande wao baadhi ya wahanga wa matukio ya uhalifu wa kutumia silaha ikiwemo tukio ambalo picha zake zimesambaa mitandaoni linalodaiwa kutokea eneo la Goba wamelishukuru jeshi la polisi kwa kufanikiwa kuwakamata wahalifu hao ambao waliwavamia na kutaka pesa kwa nyakati tofauti huku wakitumia silaha za moto kama bunduki kupora fedha.

