Back to top

SHEKHE WALID, MWAMPOSA MABALOZI UHIFADHI WA BAHARI

08 June 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema Wizara yake itawatumia Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shekhe Walid Alhad Omar na Mchungaji wa Kanisa la Arise and Shine na Boniface Mwamposa, kuwa mabalozi wa uhifadhi wa Bahari ili wasaidiane nao katika kuelimisha jamii hasa zinazoishi kando ya Bahari juu ya athari ya uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira ya Bahari kwa ujumla.

Waziri Ulega amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Bahari Duniani yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam Juni 8, 2023.

Alifafanua kuwa pamoja na uwepo wa Sheria  kwenye usimamizi na uendelevu wa rasilimali za Bahari, ni muhimu pia kushirikiana na jamii katika kuhakikisha mazingira ya Bahari yanahifadhiwa vizuri kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha jamii wameamua kuwatumia Viongozi hao wa Dini kuwa mabalozi na kuwaelimisha juu ya umuhimu wa kuepuka vitendo ambavyo vinapelekea uharibifu wa mazingira ya Bahari.

"Sisi Wizara na Kitengo chetu cha MPRU tupo tayari kushirikiana na viongozi hawa ili waweze kutusaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya athari ya Uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira"Amesema

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.David Silinde alisema kuwa pamoja na changamoto ya matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo imekuwa moja ya kisababishi cha uharibifu wa mazingira ya bahari, yeye pamoja na Waziri Ulega wamedhamiria kuhakikisha kuwa wanaendelea kusimamia  matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari ili ziendelee kuchangia vyema kwenye uchumi wa buluu.

Kiongozi mwingine wa dini atakayeshiriki kuelimisha jamii ni kutoka Kanisa Katoliki Tanzania, Padri James Ngonyani.

Kauli Mbiu ya Siku ya Bahari Duniani kwa mwaka 2023 ni 'Sayari ya Bahari'Mawimbi Yanabadilika.