
Serikali imesema imetenga shilingi bilioni mia moja kumi na mbili katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali zinazokabiliwa na uhaba wa vifaa tiba.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Deogratius Ndejembi ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe.Martha Festo Mariki aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kutatua changamoto ya vifaa tiba katika hospitali za wilaya zinazojengwa kote nchini.
Mhe.Ndejembi amesema serikali imetenga shilingi bilioni sabini na moja katika fedha hizo, kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya kinywa meno na macho katika hospitali sabini na moja hapa nchini.
Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, serikali imetenga shilingi bilioni kumi na tano nukta tano kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vya hospitali thelathini na moja zinazoendelea na ujenzi na kila moja imetengewa shilingi milioni mia tano.
Mheshimiwa serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zote nchini ili kuziwesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
