
Mchimbaji wa Madini amefariki na wengine watano wameokolewa baada ya kufukiwa na kifusi walipokuwa wakiendelea na shughuli za uchimbaji, katika Kijiji cha Rarieda Uyore huko Alego-Usonga, Kaunti ya Siaya, nchini Kenya.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Siaya, Benedict Mwangangi, amethibitisha kifo cha mchimbaji huyo mmoja ambaye hakutajwa jina lake, huku akibainisha kuwa wengine watano wameokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya ambapo watatu kati ya hao watano wametibiwa na kuruhusiwa, wachimbaji wawili wanaendelea na matibabu katika kituo hicho huku akibainisha kuwa hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda Mwangangi amesema Mwili wa mchimba aliyefariki umechukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Siaya kusubiri kufanyiwa uchunguzi.
Mwangangi amesema uchunguzi unaendelea kubaini iwapo mgodi huo wa dhahabu ulikuwa unafanya kazi kihalali ama la, na kutoa onyo kali kwa wachimbaji wa dhahabu sio tu katika kijiji cha Rarieda Uyore lakini kote Kaunti ya Siaya kuacha kuingia kwenye mashimo ya madini, haswa wakati wa usiku.
Aidha mchimbaji huyo alikuwa pamoja na wenzake sita wakati wa shughuli zao za uchimbaji madini wakati lilipo poromoka na kuwafukia.
