Back to top

DKT.SAMIA:UCHUMI WA BULUU NI FURSA

24 June 2023
Share

Rais wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema, uchumi wa buluu ni fursa, huku akiwataka wananchi kujipanga na kuweka mazingira muafaka ya uwekezaji ili waweze kunufaika kupitia rasilimali zinazopatikana katika sekta hiyo.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema maana halisi ya uchumi wa buluu ni matumizi endelevu ya rasilimali zilizomo kwenye bahari, maziwa na mito kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa, kutengeneza ajira na kuleta ustawi wa maisha ya watu na vilevile kutunza afya ya maumbile ya bahari.

Dkt.Samia alisema hayo katika sherehe za Msimu wa Pili wa Tamasha la Vyakula vya Baharini (Zanzibar Sea Food Festival) lililofanyika katika ufukwe wa Kendwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.

Amesema kupitia tamasha hilo ni muhimu kujizatiti na kujipanga vyema ili kuweza kuzitumia fursa zilizopo na zinazojitokeza katika sekta ya uchumi wa buluu.

Ameongeza kwa kusema kuwa ili fursa hizo ziweze kuwa endelevu ni muhimu kuhakikisha kunakuwa na mipango ya matumizi sahihi ya bahari, usimamizi bora wa ikolojia za bahari, kudhibiti uchafuzi wa bahari, kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na kusimamia mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini na kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya usimamizi bora wa uchumi wa buluu na rasilimali zake.

Ameeleza kuwa ni muhimu kuweka kipaumbele kwenye hifadhi ya mazingira ya bahari kwani bila kufanya hivyo hakutakuwa na upatikanaji endelevu wa samaki na mazao mengine ya bahari.

Aidha, amebainisha kuwa mipango ya maendeleo ya Kitaifa imeagiza kutekeleza ajenda ya uchumi wa buluu ya Tanzania, kama ilivyoainishwa kwenye Mpango wa (Vision) 2050 kwa Zanzibar na Dira ya Maendeleo ya 2025 kwa Tanzania.

Halikadhalika, amesema kuwa kufuatia fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ambazo zinaweka uhakika wa Chakula nchini, ni vyema Watanzania wakajipanga kupitia Jukwaa la mifumo ya Chakula Afrika linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 5 - 8, 2023 ili nchi yetu iweze kulilisha Bara la Afrika kwa mazao ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.