
Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaandaa sera itakayowezesha Diaspora kuwekeza katika ujenzi na kununua nyumba, zitakazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa na waendelezaji wengine.

Hayo yamebainishwa mkoani Dar es Salaam, na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, wakati wa kuabidhi nyumba 43 pamoja na maeneo 49 ya biashara kwenye Mradi wa Morocco Square unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Pia ametoa wito kwa watanzania waishio ughaibuni kutumia fursa ya sera ya ubia ya NHC iliyoboreshwa kuja kuwekeza katika sekta ya nyumba.‘’Uwekezaji huu uwe ni wa nchi nzima na siyo Dar es Salaam pekee kwa kuwa NHC inayo viwanja na majengo yaliyopitwa na wakati katika miji yetu mbalimbali nchini’’. Alisema Dkt Mabula
Akielezea zaidi kuhusu Mradi wa Morocco Square, Dkt Mabula alisema mradi huo ni kielelezo cha uboreshaji wa miji kwa kuondoa majengo machakavu na yaliyopitwa na wakati na kujenga majengo makubwa ya kisasa.
Akigeukia suala la ununuzi wa nyumba za mradi huo, Dkt Mabula ameshauri taratibu za kupata hati pacha za umiliki (Unit title) ufanyike mapema kwa kuwa ndiyo salama ya milki pamoja na uwezesho katika shughuli za maendeleo.
Ametoa rai kwa wapangaji kutunza miundombinu katika jengo hilo ili kuendelea kulinda umaridadi wa uwekezaji uliopo katika viunga vya morocco square.
Hata hivyo, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka taratibu zote baada ya hatua za ujenzi kukamilika ili wahusika wapate fursa ya kutumia hati zao kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo kupata mikopo benki.
Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdalah amesema, walionunua na kupangisha nyumba katika mradi wa Morocco Square wako katika maisha tofauti kwa kuwa mradi huo ni ghali kuliko kuliko miradi yote inayotekelezwa na shirika lake kutokana na kuwa na vifaa vyenye ubora wa hali ya juu.
Mmoja wa wateja wa NHC Abouubakar Aboubakar ameishukuru serikali pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuweza kufanikisha mradi huo na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo.
