
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake imejipanga kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo mkoani Morogoro kwa kuanzisha programu maalum ya kuwawezesha vijana na wafugaji wengine kufanya ufugaji wa kibiashara na kuifanya sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa wa kipato kwa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Ulega amesema hayo wakati akiongea na Viongozi wa Mkoa wa Morogoro katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Amesema Mkoa wa Morogoro una fursa nyingi zinazoweza kuinua uchumi wa Wana Morogoro kwa kutumia uzalishaji wa mifugo ikiwemo ardhi nzuri inayowezesha kupatikana kwa maji ya uhakika na malisho kwa mifugo.
Amebainisha kuwa mpango wa Wizara ni kutumia maeneo ya Ranchi za Taifa (NARCO) kupangisha vijana na wafugaji kwa muda maalum ambao utawawezesha wafugaji kutumia eneo kwa muda mfupi kufanya unenepeshaji wa mifugo na kisha kuiuza ndani na nje ya nchi.
“ Mhe. Mkuu wa Mkoa, Wizara yangu imepanga kutenga eneo lenye ukubwa wa hekta 10,000 kutoka kwenye Ranchi mama kwa ajili ya Vijana waliomaliza mafunzo kwenye vituo atamizi na Wafugaji wa Mkoa wa Morogoro ambao wanahitaji maeneo ya malisho (Livestock Guest House) kwa ajili ya kufanya unenepeshaji wa mifugo", amesema
Ameafanua kuwa katika maeneo hayo watakayoyatenga kwa ajili ya kupangisha wafugaji kwa muda mfupi wataiwekea miundombinu kama vile majosho, mabwawa, mabilika, mazizi, ghala la majani na nyumba maalum ya mifugo.
Aidha, ameongeza kuwa serikali itaendelea kutoa elimu ya uwekezaji kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Mifugo kwa Wadau wote wakiwemo wafugaji huku akiwataka wafugaji kumiliki maeneo kwa ajili ya mifugo yao.
Halikadhalika, amesema ili kukabiliana na migogoro, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na Wadau wa Sekta ya Mifugo imepanga kumega jumla ya hekta 27,006.27 kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa vijiji vya Twatwatwa, Parakuyo, Ngaite, Tindiga A na B, huku akisisitize kuwa maeneo hayo yagawiwe vizuri na yatumike kwa shughuli zilezile za Mifugo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima alisema kuwa ana imani kubwa na wizara na aliiomba wizara kuingia makubaliano rasmi na mkoa huo katika kufanya programu za ufugaji wa kibiashara ili wananchi wa mkoa huo wanufaike na ufugaji na kuepuka migogoro isiyo na tija.
Aliongeza kuwa wanataka kuanzisha vituo vya BBT mifugo mkoani humo vingi iwezekanavyo ili vijana na wafugaji wengine wapate elimu ya ufugaji wa kibiashara waweze kujikwambua kimaisha.
