
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, amesema uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika mwaka ujao kama ilivyopangwa na kwamba atawania Urais.
Salva Kiir, Kamanda Mkuu wa wapiganaji wa msituni, amekuwa rais pekee wa taifa hilo tangu alipoliongoza kupata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
"Ninakaribisha uidhinishaji wa kugombea urais mwaka 2024," Kiir aliwaambia wafuasi wa chama chake tawala cha Sudan People's Liberation Movement, akilielezea kama "tukio la kihistoria."
Tangazo la Rais Salva Kiir la kufanyika kwa uchaguzi limeleta matumaini kwa wananchi waliokuwa wakiusubiri kwa shauku kubwa.
Amesema uamuzi wake wa kuwania, urais umetokana na kuungwa mkono wa chama chake cha Sudan People's Liberation Movement - SPLM.
Hakuna mwanasiasa mwingine ambaye ametangaza nia yake ya kugombea, lakini hasimu wake wa muda mrefu, Riek Machar, anatarajiwa kugombea.
