
Halmshauri Kuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kusini Unguja imemfuta uanachama kada wake Balozi Ali Karume.
Taarifa ya kumuondosha kwenye chama hicho ilitolewa na Katibu Mwenezi wa Mkoa huo, Ali Timamu Haji, kutokana na kikao kilichofanyika saa saba usiku wa kuamkia leo Julai 8, 2023 chini ya Katibu wa Mkoa wa CCM, Amina Mnacho.
Hatua hiyo inakuja baada ya chama hicho kumpa onyo kutoka na kauli zake akidaiwa kukidhalilisha chama hicho.
"Mwanachama huyu ameitwa na kuonywa kwa maandishi na vikao mbalimbali vya Chama Cha Mapinduzi, lakini hakutii wala kubadilisha tabia na vitendo vyake na kuendelea kukiuka kwa makusudi maadili na miongozo ya CCM hivyo kwa mamlaka tuliyopewa na Katiba yetu ngazi ya Mkoa ya CCM Kusini Unguja kwa kauli moja tumefikia maamuzi makubaliano ya kumuachisha na kumfukuza uanachama mwanachama huyo"Amefafanua Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja.
Mwanachama na mwanasiasa mkongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya,Mkoa,Mwakilishi wa kuteuliwa,Waziri Mstaafu wa Mawasiliano,ujenzi na Uchukuzi Zanzibar,Waziri wa Vijana na Michezo Zanzibar pamoja na kuwa Balozi Mstaafu wa Tanzania mwaka 2006.
