
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewakumbusha Wasimamzi wa Uchaguzi kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba ajira za watendaji wa uchaguzi zinazingatia sifa na uwezo.
Ukumbusho huo umefanywa na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa), Mbarouk Salim Mbarouk mkoani Morogoro Agosti 10, 2023, wakati akifunga mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maafisa uchaguzi.
Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu na kuhudhuriwa na washiriki 88 ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara.
Aidha, amewahimiza watendaji wa uchaguzi kutenga muda kujisomea ili kupata ufahamu wa sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023, wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023.
Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
