Back to top

HATIMILIKI 420 ZA ARDHI HAZIJACHUKULIWA KLM

14 August 2023
Share

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amebaini zaidi ya hatimiliki za ardhi 420 za wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro hazijachukuliwa hadi sasa na wahusika.

Pinda amebaini hayo wakati alipofanya ziara katika Ofisi ya Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro, na kubaini ofisi hiyo imeandaa hatimiliki za ardhi zaidi ya 420 ambazo wamiliki wake hawajazichukua hadi sasa.

Pinda amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Kilimanjaro Bw.Leonard Msafiri, kwa kushirikiana na Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro Bibi Esther Shayo, kufanya matangazo ya kutosha ili wamiliki wa hati hizo wafike katika ofisi ya Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Kilimanjaro na kuzichukua hati zao.

Aidha, Pinda amewataka watumie njia mbalimbali za matangazo ikiwemo redio za kijamii, Luninga na mbao za matangazo katika ofisi za Serikali mkoani Kilimanjaro ili taarifa ziwafikie walengwa kwa urahisi popote walipo.